Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha inawafikia wananchi popote walipo na kuwapatia huduma muhimu za ardhi.
Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za ardhi kwa urahisi, haraka na karibu na maeneo wanayoishi, pamoja na kupunguza usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Akizungumza Machi 4, Iringa wakati wa uzinduzi wa Samia Ardhi Kliniki, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Kaspar Mmuya alisema maelekezo ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ni kuhakikisha wananchi wanafikiwa kwenye makazi yao na kupewa huduma zinazohusu ardhi.
“Maelekezo ya Dk Mwigulu Lameck Nchemba ni kwamba wafuateni watu waliko mkasikilize kero zao,” alisema Mmuya.
Aliongeza kuwa wataalamu wa ardhi kote nchini wanawajibu wakutumia majukwaa ya mikutano mbalimbali ya viongozi wa Serikali kutoa elimu kwa wananchi ili kujenga uelewa wa pamoja katika sekta ya ardhi, pia wataalamu hao kuanza kutoa elimu ya ardhi kwa wananchi.
