Clement Shawishi- GEITA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Hamad Masauni ameagiza Tume ya Usimamizi wa Mazingira NEMC kuelimisha wachimbaji wadogo kuhusu athari za matumizi ya kemikali ya zebaki kwenye shughuli zao.
Mha. Masauni ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake Mkoani Geita kwaajili ya kukagua ujenzi wa Ofisi za NEMC zitakazohudumia Mikoa ya Geita, Shinyanga na Mara
Amesema NEMC haina budi kutafuta teknolojia mbadala kwa kushirikiana na Taasisi za Kimataifa ili kutunza mazingira na kuimarisha shughuli za uchimbaji madini bila kuathiri afya za wananchi
Mratibu wa ujenzi wa Ofisi hizo za NEMC Mkoani Geita Mhandisi Befrina Iguli amesema kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na NEMC tani 18 mpaka 22 za kemikali ya Zebaki hutumiwa na wachimbaji wadogo katika uchenjuaji

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema kiwango kikubwa cha matumizi ya Zebaki katika uchenjuaji ni changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo licha ya Mkoa kuanzisha kampeni ya upandaji miti kila mwaka kurejesha uoto wa asili ulioathiriwa na shughuli za uchimbaji madini
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Emaculata Sware ameeleza kuwa ujenzi wa Ofisi hizo unagharimu Dola za Kimarekani Milioni 3.8 na utekelezaji wake mpaka sasa umefikia asilimia 80.
