Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ametoa wito kwa wadau wa elimu nchini kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo Mkakati na Miongozo ya Kitaifa ya matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu, akisisitiza kuwa hatua hiyo ndiyo msingi wa mageuzi ya elimu nchini.
Akizungumza katika warsha ya kujenga uelewa kwa wadau juu ya Mkakati huo, leo Januari 14, 2026 Jijini Dodoma Prof. Nombo alisema mkakati huo unaweka mfumo wa kitaifa wa pamoja utakaoratibu na kuongoza mageuzi ya kidijitali katika ngazi zote za elimu kuanzia shule, vyuo vya ualimu, elimu na mafunzo ya ufundi stadi (TVET), vyuo vikuu, hadi mifumo ya ujifunzaji isiyo rasmi.
Amesema kwa shule, vyuo vya ualimu, taasisi za TVET na vyuo vikuu, utekelezaji unapaswa kuanzia kwenye kuimarisha misingi ya kidijitali, ikiwemo upatikanaji wa intaneti, mitandao ya ndani ya taasisi, vifaa vya kidijitali, vyanzo vya umeme vya kuaminika pamoja na matumizi thabiti ya majukwaa ya kujifunzia mtandaoni na mifumo iliyoidhinishwa.
Aidha, amewahimiza washirika wa maendeleo kuhakikisha misaada yao inalingana na Mkakati wa Kitaifa wa Elimu ya Kidijitali, kwa kuzingatia athari za kimfumo, ujenzi wa uwezo na uendelevu.
Kwa upande wa sekta binafsi na wabunifu wa teknolojia (EdTech), amewataka kuendelea kubuni kwa pamoja suluhisho zinazojibu mahitaji ya nchi, sambamba na kuzingatia viwango vya kitaifa, misingi ya kimaadili na ulinzi wa data.
Prof. Nombo amebainisha kuwa usambazaji wa vifaa pekee hautoshi, akisisitiza kuwa utekelezaji madhubuti unahitaji uongozi, uratibu, rasilimali na uwajibikaji katika ngazi zote. Amezitaka taasisi za elimu kuingiza mkakati huo katika mipango yao, kuteua waratibu, kutenga rasilimali na kushiriki kikamilifu katika ufuatiliaji, tathmini na kujifunza kwa pamoja.