
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Bodi ya Nyama Tanzania imesema imeendelea kutekeleza mkakati wa kukuza mauzo ya nyama nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza fedha za kigeni.
Hayo yamebainishwa na Dkt. Ashatu Kijaji leo Mei 23, 2025 Bungeni Jijini Dodoma, wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya wizara ya Mifugo na uvuvi kwa mwaka 2025/26.
Dkt. Kijaji amesema hadi kufikia Aprili mwaka huu, tani 9,863.41 za nyama zenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.7 zimeuzwa sawa na asilimia 89.9 ya lengo la kuuza tani 10,971 ikilinganishwa na tani 9,326.3 zenye thamani ya Trilioni 3.4 zilizouzwa kipindi kama hicho Mwaka 2023/2024.
Kulingana na Dkt. Kijaji, ongezeko hili ni sawa asilimia 5.75, likitokana na jitihada zinazofanywa na serikali kwa kuongeza ushirikiano na fursa za kibiashara nje ya nchi hali iliyopelekea masoko ya nyama kuendelea kuongezeka kufikia nchi 11 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.
Katika hatua nyingine Dkt. Kijaji amesema kwa Mwaka 2025/2026, Wizara yake itaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuwezesha Vijana kujiajiri kwa kuwekeza katika shughuli za ufugaji, uvuvi na ukuzaji viumbe maji kupitia Programu ya BBT ambapo Vijana 440 watawezeshwa kujiajiri ikiwemo kupewa mitaji.