
Mahakama ya wilaya ya Kakonko, imewatia hatiani Bw. Onesmo Janks Nimbuga (34) ambaye ni muuguzi mkunga katika kituo cha afya Mtendeli Pamoja na Bi. Annie Newton Mabago (37) aliyekuwa mganga mfawidhi wa kituo hicho kwa makosa ya 22 ya rushwa na uhujumu uchumi.
Makosa hayo 22 ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri 28(1) Ubadhirifu na Ufujaji Kinyume na Vifungu vya 22 na 28(1) vyote vya sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, Pamoja na Kughushi kinyume na kifungu cha 333, 335(a) na 337 vya Kanuni za adhabu sura ya 16 marejeo ya 2022.
Washtakiwa hao wakiwa katika kituo cha Afya Mtendeli walifanya malipo hewa kwa kuandaa hati ya malipo na kughushi kuonyesha kuwa walinunua betri ya sola N200 yenye thamani ya shilingi 586,200/= na badala yake walitumia kiasi hicho cha fedha kwa matumizi yao binafsi.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko Ambilike Kyamba na kuendeshwa na mwendesha mashtaka wa Serikali kutoka Ofisi ya TAKUKURU (M) Kigoma Bw. Jackson Lyimo, washtakiwa wamehukumiwa kulipa faini ya kiasi cha Tshs. 1,000,000/= na kurejeshwa kiasi cha Tshs. 586,200/= kilichofanyiwa ubadhirifu katika akaunti ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), jambo ambalo limetekelezwa na washtakiwa.