
Katika mataifa mengi ya Afrika, kilimo cha ndizi kina mchango mkubwa katika maisha ya jamii, lakini baadhi ya matukio yanayotokea mashambani yanazua sintofahamu na imani tofauti.
Mojawapo ni hali isiyo ya kawaida ya mgomba mmoja kuzaa mikungu miwili au mitatu.
Tukio hili, ambalo wataalamu wanalichukulia kama hali isiyo ya kawaida ya kibayolojia, limejawa na tafsiri nyingi za kitamaduni na kiimani. Baadhi ya jamii hulitazama kama ishara ya baraka na neema, wakiamini kuwa linaashiria mafanikio, ustawi, na hata uwezekano wa kupata watoto mapacha. Wanaamini kuwa kula ndizi hizo huleta bahati njema.
Hata hivyo, upande mwingine wa shilingi unatafsiri tukio hili kama ishara ya nuksi au balaa. Kwao, mgomba wa namna hii huashiria bahati mbaya inayoweza kumpata mkulima au familia yake. Kutokana na imani hii, baadhi ya wakulima huukata mgomba huo mara moja na kuzuia ndizi zake zisiliwe na mtu yeyote, wakiamini kuwa matunda hayo yanaweza kuleta madhara.
Ingawa mtaalamu mmoja wa kilimo kutoka Tanzania aliiambia Radio Kwizera kuwa hali hiyo inaweza kusababishwa na ukame mkali, bado utafiti zaidi unahitajika ili kubaini chanzo chake kisayansi.
Swali linabaki kuwa: Je, mgomba kuzaa mapacha ni jambo la kawaida au ni tukio lenye tafsiri za kipekee kulingana na jamii husika?
Je, katika eneo lako hali kama hii inatafsiriwa vipi? Tujulishe maoni yako katika sehemu ya maoni.