Shirika la Miss Universe Jamaica limetoa taarifa rasmi kuhusu hali ya kiafya ya Gabrielle Henry “Gabby”, aliyelazwa nchini Thailand baada ya kuanguka jukwaani wakati wa mashindano ya Miss Universe 2025.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dada yake Gabrielle, Dkt. Phylicia Henry-Samuels aliye Thailand pamoja na mama yao, Maureen Henry ameeleza kuwa hali ya Gabrielle si nzuri kama walivyotarajia, ingawa madaktari wanaendelea kumpa matibabu ya karibu.
Madaktari wamethibitisha kuwa Gabrielle atalazimika kuendelea kuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa angalau siku saba, ili kufuatiliwa kwa umakini na kupatiwa matibabu maalum.
Katika taarifa hiyo, Miss Universe Jamaica Organization imewaomba Wajamaica na watu wote duniani kuendelea kumwombea Gabrielle, wakisisitiza umuhimu wa upendo, nguvu na matumaini katika kipindi hiki kigumu kwa familia yake
Shirika hilo pia limewataka mashabiki na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza taarifa potofu, maneno hasi, au uvumi unaoweza kuongeza msongo wa mawazo kwa familia ya Gabrielle.
Taarifa hiyo imehitimisha kwa kusisitiza kuwa kipaumbele cha sasa ni afya ya Gabrielle na ustawi wa wapendwa wake, huku familia ikiomba heshima, faragha na huruma wakati wakipitia kipindi hiki cha changamoto.