Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imepata pigo kabla ya mechi zijazo za mashindano ya FIFA Series baada ya mshambuliaji, Simon Msuva kuondolewa kikosini kutokana na changamoto ya usafiri Mashariki ya Kati kutoka na mgogoro baina ya Iran dhidi ya Marekani na Israel.
Msuva, anayechezea Al-Talaba SC inayoshiriki Ligi Kuu Iraq, ameshindwa kujiunga na kikosi hicho, jambo lililomlazimu kocha mkuu Miguel Gamondi kufanya mabadiliko ya ghafla kwenye safu ya ushambuliaji.

Gamondi amethibitisha kuwa juhudi za kumpata mshambuliaji huyo hazikufanikiwa, hivyo kuamua kumchukua Morice Abraham wa Simba SC kama mbadala wake.
โTulifanya kila liwezekanalo kuhakikisha Msuva yupo kwenye kikosi, lakini haikuwezekana kutokana na hali ilivyo sasa. Tumemjumuisha Morice Abraham ili kuimarisha timu,โ amesema Gamondi.
Licha ya changamoto hiyo, maandalizi ya mashindano yanaendelea, ambapo tayari timu imefanya mazoezi ya kwanza jijini Dar es Salaam kabla ya kuondoka kuelekea Kigali, Rwanda leo, Jumanne, Machi 24, 2026.
