Clement John- GEITA
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Shabaka iliyopo Kata ya Shabaka Wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita Mwl. Maziko Reuben amesema kukamilika kwa ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa shuleni hapo kutapunguza utoro wa wanafunzi shuleni na kuimarisha ufaulu wao kitaaluma.
Mwl Reuben amesema hayo baada ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Nyang’hwale kuzuru shuleni hapo kukagua mradi huo unaotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu kupitia mradi wa BOOST.
Amesema ujenzi wa mradi huo umesaidia kutoa fursa za ajira kwa wakazi wa Kakola, Shabaka na maeneo mengine ambapo umehusisha pia ujenzi wa vyoo na jengo la Utawala.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Wilaya ya Nyang’hwale Bw. Said Madoshi ameeleza kuridhishwa na uaminifu wa Kamati inayosimamia ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa na Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Nyang’hwale Bw. Alhaj Adam Mtore amepongeza Uongozi wa Shule na Kamati ya Usimamizi wa ujenzi kwa kuzingatia ubora wa majengo kwenye miradi ya Umma kulingana na Ilani ya CCM.
Mradi huo wa ujenzi wa Shule ya awali na msingi Shabaka unagharimu Milioni 330.7 na kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 80.

