Shafiru Yusuph- Muleba, KAGERA
Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera leo Aprili 02, 2026 imesaini mkataba wa ujenzi wa jengo jipya la utawala lenye thamani ya shilingi bilioni 6, mradi ambao utakelezwa na kampuni ya SUMAJKT Construction Company Ltd.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Bw. Magongo Justus, amemtaka mkandarasi kuandaa mpango kazi madhubuti na unaotekelezeka ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa viwango vinavyotakiwa.
Bw. Magongo amesisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu wa mradi huo kwa kuhakikisha kuwa kila hatua ya ujenzi inazingatia ubora unaotakiwa, sambamba na kutumia rasilimali kwa ufanisi ili kuleta thamani halisi ya fedha za Serikali katika mradi huo.

Naye Meneja wa Kanda ya Ziwa Magharibi wa SUMAJKT Construction Company Ltd, Meja Hamadi Matata, ameihakikishia halmashauri kuwa watatekeleza mradi huo kwa ubora wa hali ya juu na kuhakikisha unakamilika ndani ya muda wa mwaka mmoja kama ilivyokubaliwa katika mkataba.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya kiutawala katika ngazi za halmashauri.

