Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamemchangua Bw. Mussa Azzan Zungu Mbunge wa Jimbo la Ilala kuwa spika wa bunge hilo.
Uchaguzi huo umefanyika leo Novemba 11, 2025, katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma, ambapo Zungu amewashinda wagombea wengine watano waliokuwa wakipeperusha bendera za vyama vyao kwa kupata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa, ambapo kura tatu ziliharibika.
Wagombea hao ni Bi. Anita Alfani Mgaya wa Chama cha NLD amepata kura moja, Ndonge Saidi Ndonge kutoka AAFP amepata kura moja, na Yeronika Charles Tyeah kutoka NRA amepata kura 0.
Wengine ni Chrisant Nyakitita kutoka DP, amepata kura 0 na Amin Alfred Yango kutoka ADC amepata kura 0.
Zungu atakuwa kiongozi wa Mhimili huo katika Bunge la 13 ambalo limeanza rasmi leo.
Aidha Zungu amekuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 20 hadi sasa, ambapo aliingia bungeni rasmi mwaka 2005, ambapo kwa kipindi hicho amekuwa Mwenyekiti wa Bunge 2012-2021 na Naibu Spika 2022mpaka 2025 na amefanya kazi na Maspika wa Bunge wanne.
Kwa Upande wa Elimu Zungu ni mhandisi wa wa Ndege na amepata mafunzo hayo nchini Tanzania pamoja na nchini Canada ambapo alihitimu mwaka 1982 na amekuwa pamoja na shahada nyingine za maswala ya Diplomasia ambazo alihitimu mwaka 2007 na mwaka 2021.