
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinafanyika kwa kistaarabu.
Akizungumza leo, katika Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa Viongozi wa Kitaifa wa Vyama vya Siasa yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), mkoani Dar es Salaam, Jaji Mutungi amesisitiza kuwa vyama vya siasa vina wajibu wa kuendeleza misingi ya amani na mshikamano wa taifa.
Ameongeza kuwa amani na mshikamano ni urithi ulioachwa na waasisi wa taifa, hivyo viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi.
Aidha, amewataka viongozi kutokubabaishwa na upotoshaji unaoweza kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii na makundi mengine katika jamii akisisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.