Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza mamlaka husika kumfukuza kazi na kumvua hadhi ya utabibu muuguzi mmoja mkoani Tabora anayedaiwa kufanya upasuaji wa mgonjwa nyumbani kwake kinyume na maadili.
Akizungumza na wafanyabiashara jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa mtumishi huyo akamatwe na kufikishwa mbele ya sheria, akibainisha kuwa Serikali imejenga miundombinu ya kutosha ya afya ili kutoa huduma salama kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Geita kuchunguza ubadhirifu wa fedha katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Nyang’wale.
Amesema kuwa amepokea taarifa za mianya ya ufisadi inayohusisha mafundi na makandarasi wanaopanga kugawana fedha za umma, hivyo anahitaji taarifa kamili ili kuchukua hatua dhidi ya wanaotanguliza maslahi binafsi.
Kuhusu ustawi wa wafanyabiashara, Waziri Mkuu amewapa viongozi wa Soko la Machinga Dodoma mwezi mmoja kukamilisha uchaguzi wa uongozi mpya ifikapo Aprili 4, 2026.
Pia, amebainisha kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza asilimia tano kwenye mfuko wa mikopo ya Halmashauri katika bajeti ijayo ili kuboresha miundombinu ya masoko nchini.
