Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amewataka viongozi na watendaji wa ngazi za Mikoa na Wilaya kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Nishati katika kusimamia utekelezaji wa Mradi wa Upelekaji Umeme katika vitongoji 9,009 nchini, ili kuhakikisha unatekelezwa kwa ufanisi na kuwanufaisha wananchi.
Ndejembi ametoa kauli hiyo Januari 22, 2026 jijini Dodoma wakati wa Mkutano Maalum wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa mwaka wa fedha 2024/2025, uliohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Lishe wa Mikoa.
Amesema mradi huo unagharimu zaidi ya Shilingi trilioni 1.5, fedha zinazotokana na walipa kodi wa Tanzania, hivyo kuna wajibu wa pamoja wa kuhakikisha zinatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
“Mradi huu unatekelezwa kwa fedha za Watanzania, hivyo tuna wajibu mkubwa wa kuusimamia kikamilifu. Mafanikio yake yanategemea ushirikiano wenu kama waratibu wa sekta zote katika maeneo mnayoyasimamia,” amesema Ndejembi.
Aidha, amewakumbusha viongozi hao kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, la kuhakikisha shule zote, vituo vya afya na zahanati zinafikishiwa umeme kupitia mradi huo, hata kama zipo nje ya umbali wa mita 30 kutoka kwenye miundombinu ya mradi.

Kuhusu gharama za kuunganisha umeme vijijini, Waziri Ndejembi amefafanua kuwa ni shilingi 27, 000 kwa wananchi waliopo ndani ya mita 30 ya mradi, wakati wa utekelezaji na hadi ndani ya miezi mitatu baada ya kukamilika kwa mradi.
Kutokana na hilo, amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na Halmashauri kuwahamasisha wananchi kutumia fursa hiyo mapema.
Hata hivyo, ili kuharakisha uunganishaji wa umeme, Waziri Ndejembi ameelekeza kuwa hata wananchi ambao hawajakamilisha utandazaji wa nyaya katika nyumba zao (partial wiring) waingiziwe umeme bila kusubiri ukamilishaji wa nyumba nzima.