
Mitandao ya kijamii imetikisika tena baada ya bilionea na mwanasiasa wa Nigeria, Prince Ned Nwoko, kumtuhumu mke wake, Regina Daniels, kwa kile alichokiita vurugu na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na pombe.
Tukio hili limeibuka siku moja tu iliyopita kupitia chapisho la video kwenye ukurasa wake wa Instagram lililovuta hisia za maelfu ya mashabiki.
Katika maelezo yake, Nwoko anadai kwamba Regina hakuwa hivi mwanzo, akisema tatizo hilo limeharibu utulivu wa familia yao.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha saa 48, Regina aliharibu mali, kuwapiga wafanyakazi watatu wa nyumbani, na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba bila sababu ya msingi.
Ned, ambaye pia ni seneta na mmoja wa wanaume tajiri zaidi nchini Nigeria, amemtaja mtu anayeitwa Sammy kama muuzaji mkuu wa dawa kwa Regina, na Ann kama mtu mwingine anayehusishwa na kile alichokiita mzunguko wa maovu.