Mamlaka ya ukuzaji wa zao la kahawa nchini Burundi (ODECA) imewapa wahusika wote wa malipo ya wakulima wa kahawa kipindi cha wiki moja kuhakikisha wamewalipa wakulima fedha zao za msimu uliopita.
Agizo hilo linazihusu Benki na taasisi za kifedha ikiwemo Lumicash ambazo zimetakiwa kutekeleza malipo hayo kote nchini.
Akizungumza jijini Bujumbura jana na wadau wa sekta ya kahawa, Mkurugenzi wa ODECA nchini Burundi Bw. Oscar Uwikunda amesema hatua hiyo inalenga kumaliza madai ya wakulima ya ucheleweshaji wa malipo yao.
Bw. Uwikunda amebainisha kuwa hadi sasa wakulima wa kahawa wameshalipwa asilimia 81 na kuagiza asilimia 19 iliyobaki iwe imewekwa kwenye akaunti za wahusika kufikia Jumanne ya wiki ijayo.