Aliyewahi kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa kwenye majukwaa ya urembo duniani, Olivia Yacé mrembo kutoka Côte d’Ivoire (Ivory Coast), ametangaza kujiuzulu rasmi nafasi yake kwenye Miss Universe uamuzi uliosababisha gumzo kubwa mtandaoni na mijadala mikali barani Afrika.
Kupitia ujumbe wake, Olivia ameeleza kuwa ameacha taji lake ili kubaki mwaminifu kwa maadili yake binafsi, kuheshimu misimamo yake kuhusu utu, heshima na stahili, na kuendelea kulipa kipaumbele jukumu lake la kuwatumikia Waafrika. Anasisitiza kuwa nafasi za uongozi, hasa katika majukwaa ya kimataifa, hazina maana ikiwa hazilingani na misingi ya heshima na uadilifu anaoamini.
Olivia Yacé, aliyekuwa ameteuliwa kuwa Miss Universe Africa & Oceania, amefafanua kuwa malengo yake sasa ni kutumia sauti yake, uwezo wake na ushawishi wake kuendeleza bara la Afrika, kulinda thamani za kitamaduni na kutengeneza fursa kwa kizazi kipya.
Uamuzi wake umepongezwa na watu wengi, wakimtaja kama mfano wa “uongozi wenye maadili” katika dunia inayokabiliwa na shinikizo la umaarufu na maslahi ya kibiashara. Kwa upande mwingine, mashabiki wameonyesha kusikitishwa lakini pia wameheshimu msimamo wake thabiti.
Olivia anaamini kuwa ni wakati wa Afrika. Ni lazima tusimame kwa utu, heshima na misingi inayojenga kesho bora.