Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Iddi Seif Bakari, amekutana na wamiliki wa kampuni za uzalishaji nguo katika makao makuu ya Jumuiya ya wenye viwanda na wafanyabiashara nchini Uturuki (MÜSİAD) jijini Istanbul, kwa lengo la kunadi fursa za uwekezaji katika sekta ya pamba nchini.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uhusiano wa Kidiplomasia wa MÜSİAD, Osman Önügöre, pamoja na wadau kutoka kampuni mbalimbali zinazojihusisha na uzalishaji wa nguo na uongezaji thamani katika mnyororo wa zao la pamba.
Akizungumza katika kikao hicho, Balozi Bakari ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania imeendelea kuboresha uzalishaji wa zao la pamba kupitia usambazaji wa mbolea, upatikanaji wa mbegu bora na kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji.
Hata hivyo Ametaja pia uwepo wa maeneo maalumu ya kiuchumi kama nyenzo muhimu ya kuendeleza viwanda, kukuza ajira na kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
