Msanii na mbunifu Pharrell Williams, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kutoa kauli nzito kuhusu siasa na namna zinavyoathiri umoja wa watu.
Akiwa kwenye mahojiano, Pharrell alitoa mtazamo wake kwamba siasa sio mfumo wa ukweli bali ni aina ya “mazingaombwe,” yaani ujanja wa kuonyesha kitu kinachoonekana halisi wakati kiuhalisia kimejengwa juu ya taswira ya uongo na ushawishi.
Anasema siasa ndivyo zilivyo, zinawagawa watu kimakusudi kwa kuwafanya wachague pande mbili zinazopingana, huku zikitumia mgawanyiko huo kuendeleza malengo ya walio juu ya mfumo.
Pharrell anaamini kuwa kuunga mkono upande wowote wa siasa ni kushiriki kwenye mgawanyiko, hata bila kukusudia.
Kwa mtazamo wake, jamii inahitaji uhuru wa kufikiri nje ya boksi, badala ya kulazimishwa kuishi ndani ya nadharia za ‘sisi dhidi ya wao’.
Pharrell anaendelea kusisitiza kuwa umoja wa watu unapaswa kuwa juu kuliko pande za kisiasa, na anataka jamii ione kwamba mara nyingi siasa ni mchezo wa kugeuza umakini yaani mazingaombwe ambayo mwisho wa siku yanatengeneza mgawanyiko kuliko mshikamano.