
Jeshi la Polisi Tanzania limetoa taarifa kuwa inawatafuta wahusika waliochapisha maudhui yasiyofaa katika ukurasa wake wa X.
Maudhui hayo yalianza kuonekana kuanzia asubuhi ya Mei 20, 2025, kwanza ikiwa ni maudhui ya ngono lakini pia na ujumbe za taarifa za uongo za kufariki kwa kiongozi.
Wadukuzi hao pia walihamia kwenye ukurasa wa polisi wa Youtube, maarufu kama Usalama TV na kuchapisha ujumbe huo.
Baadhi ya taasisi zingine ambazo kurasa zao zimeathirika ni pamoja na ukurasa wa Tanzania Investment Centre katika mtandao wa X, ukurasa wa timu ya Simba wa Youtube, ukurasa wa Mamlaka ya mapato (TRA Online TV) wa Youtube.
Pia ukurasa wa kampuni ya Airtel kwenye mtandao wa X na Youtube, pamoja na ukurasa wa Chama cha Mapinduzi Youtube na UN Tourism wa Youtube, na ukurasa wa Youtube wa University of Dar es Salaam.
Katika taarifa yake Polisi imeeleza kuwa inaendelea kuwafuatilia wahalifu waliotengeneza na kusambaza taarifa hizo.
Msemaji wa Serikali ametoa taarifa ya kuwataadharisha wananchi juu ya uwepo wa taarifa za upotoshaji katika mitandao ya kijamii.