
Jeshi la Polisi mkoa wa Geita limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio la Bw. Elisha Juma mkazi wa Katente tarafa ya Ushirombo wilayani Bukombe mkoani humo kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa studio.
Taarifa ambayo imetolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo imeeleza kuwa, taaria za mtu huyo zimepokelewa kwenye kituo cha polisi Bukombe Agosti 21, 2025 zikieleza kuchukuliwa kwa mtu huyo mnamo Agosti 19 katika studio inayojulikana kwa jina la MAS J iliyopo mtaa wa Kilimahewa kata ya Bulangwa saa 10:00 jioni.
Kamanda Jongo amesema Bw. Elisha Juma ambaye ni mwimbaji wa nyimbo za injili alichukuliwa na watu watatu ambao walikuwa na gari lenye rangi nyeupe ambalo usajili wake bado haujafahamika.
Amesema wakati wa tukio hilo, kulikuwa na watu wengine kwenye studio hiyo lakini hawakuweza kutoa taarifa za tukio hilo mahali popote kabla ya kuripotiwa kwenye kituo cha polisi Agosti 21.
Taarifa za kutoweka kwa mtu huyo pia zimeonekana katika mitandao ya kijamii ikiwemo facebook tangu alivyochukuliwa na watu ambao hawakujulikana
Uchunguzi wa tikio hilo umeanza kufanyika huku jeshi la polisi mkoa wa Geita likiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kutoa taarifa kuhusiana na tukio hilo ili kufanikisha kupatikana kwa mtu huyo.