Jeshi la Polisi nchini limetahadharisha juu ya kauli za uchochezi zinazoweza kupelelea uvunjifu wa amani nchini ambazo ni kali na zingine laini.
Jeshi hilo limetangaza kufuatilia kwa karibu hali ya kiusalama nchini na kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wowote wa sheria, unatokana na kauli za uvunjifu wa amani.
Onyo hilo la Jeshi la Polisi nchini, linajiri katika kipindi ambacho kumeshuhudiwa matamko kutoka kwa makundi na watu mbalimbali kufuatia vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 wakitoa kauli tofauti tofauti.
Katika taarifa iliyotolewa na Jeshi hilo leo Ijumaa Novemba 21, 2025 Makao makuu Dodoma, jeshi hilo limesema limebaini kuwepo kwa baadhi ya watu wanaotumia majukwaa mbalimbali kutoa kauli zinazoweza kuchochea mgawanyiko ndani ya jamii.
Jeshi la Polisi linafafanua kuwa kutoa kauli za kuchochea chuki na kuibua hisia za uvunjifu wa amani ni jambo linalokiuka sheria na kuhatarisha utulivu wa nchi.
Aidha, Polisi imesema aitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayejihusisha na lugha laini au kali yenye mwelekeo wa uchochezi, ikisema hatua hizo ni muhimu katika kuzuia chuki na vurugu ambazo zina athari kubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi kwa umakini kuhakikisha amani inaendelea kutawala kipindi hiki nchi inayohitaji maridhiano ili kurejesha amani kwani vurugu zikizuka, athari zake ni pana na humgusa kila mwananchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiusalama,” imesema taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini.