Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema changamoto ya uratibu wa mifumo ya elimu pamoja na matumizi hafifu ya fursa zilizopo bado inaendelea kujitokeza miongoni mwa Watanzania, hali inayohitaji maboresho ya sera na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wadau wa elimu.
Waziri Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma leo wakati wa kikao chake na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kilicholenga kujadili mwelekeo wa sekta ya elimu nchini Na kusema bado kuna haja kubwa ya kuboresha mifumo ya elimu ili iweze kuzungumza kwa pamoja kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu.
Ameeleza kuwa uratibu mzuri wa mifumo hiyo utawezesha kufahamu kwa kina changamoto zinazosababisha Watanzania wengi kushindwa kunufaika na fursa mbalimbali za ufadhili na mikopo ya masomo zinazotolewa na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Aidha katika mjadala huo, wadau wa elimu pia wameelekeza umuhimu wa upatikanaji wa taarifa za kutosha kuhusu utekelezaji wa mfumo mpya wa elimu ya msingi wa miaka sita, maboresho ya mitaala pamoja na utoaji wa tuzo za amali, ili kuhakikisha mageuzi yanayofanyika katika sekta ya elimu yanaeleweka na kutekelezwa ipasavyo.