Sanaa ya muziki wa sasa hauhesabu mafanikio kwa ukubwa wa jina pekee bali kwa namna timu ya msanii inavyosimamia mzunguko wa jinsi wimbo unavyotakiwa kuwafikia mashabiki. Hii imeonekana wazi kupitia nyimbo mbili ambazo zimegusa hisia tofauti ndani ya muda mfupi ikiwemo “Sweety” ya Nandy & Jux (views 1.5M kwa wiki 2),na “Chakacha” ya Pipijojo (views 1.1M kwa siku 3).
Nandy, akiwa ni alama ya ubora kwenye kiwanda cha muziki wa Bongo Fleva, ameendelea kuwekeza kwenye Promosheni inayoendelea kutetea jina la biashara yake. Ai Video ya “Sweety” ni mfano wa biashara yenye ubora wa kimataifa, muonekano wa kitajiri, na ujumbe wa mapenzi unaokubalika kwenye masoko mengi.
Kampeni yake ililenga kusambaa kwa haraka, pia kudumisha heshima ya Nandy.
Timu yake imejenga picha ya Nandy kama msanii mwenye kiwango cha juu cha ubunifu, aliye na ubora, anayewakilisha wanawake wapambanaji kwenye muziki wa kisasa.
Kwa upande mwingine, “Chakacha” ya Pipijojo ni somo zito kwa timu zote za wasanii wachanga. Ni mfano wa PR ya ksasa inayotumia simulizi, upekee, na ushirikiano na mashabiki wa mtandaoni kwa kiwango cha juu.
Kila kipengele cha kazi yake mavazi, mandhari ya video, hadi lugha ya mwili vinaunda utambulisho wa kipekee unaounganisha muziki na tamaduni.
Timu ya Pipijojo imeonyesha kwamba nguvu ya PR haipo kwenye bajeti peke yake, bali kwenye uamuzi sahihi, ubunifu, na kujua unataka masabiki wako wajisikieje.
Huu si ushindani kati ya Nandy na Pipijojo, bali ni ushahidi wa nguvu ya PR bora katika nyakati za kidigitali. Nandy anaonyesha thamani ya ubora kwa uzoefu, wakati Pipijojo anaonyesha uwezo wa kizazi kipya kutumia mitandao kama jukwaa la simulizi na si matangazo tu.
Kwa pamoja, wanatufundisha kwamba muziki mzuri hauhitaji Bahati, unahitaji kampeni zilizopangiliwa kimkakati.