Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia raia 14 wa Burundi waliokamatwa wakiwa wameingia nchini kinyume na sheria kwa kutumia usafiri wa magari mawili tofauti ya abiria.
Taarifa ya kukamatwa kwa raia hao imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, Novemba 23, 2025 Wilaya ya Sengerema wakati akizungumza na vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, mafanikio ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao yametokana na ufuatiliaji wa mienendo ya kihalifu na uwekaji wa vizuizi barabarani: Katika Kijiji cha Busisi, Tarafa ya Sengerema, ambapo jumla ya raia wa Burundi 13 walikamatwa Novemba 23, 2025 majira ya 7.30 mchana wakiwa wanasafiri ndani ya gari aina ya Tata yenye namba za usajiri T. 337 DYA, mali ya Chiza Francis Lugubi, mkazi wa Dodoma, linalofanya safari zake kati ya Kabanga (Ngara, Kagera) na Mwanza.
Wakati wa kukamatwa, dereva wa gari hilo, aliyetambulika kwa jina la Jonas Richard, alifanikiwa kutoroka eneo la tukio na jitihada za kumsaka zinaendelea.
Watuhumiwa wengine waliohusika katika kuwasafirishaji raia hao ni pamoja na Mustahper Emily miaka 24, fundi magari mkazi wa Kahama, Shinyanga na Pendo Matembere miaka 36 kondakta mkazi wa Nyegezi, Mwanza.

Baada ya kuhojiwa, ilibainika kuwa watuhumiwa hao waliingia nchini kupitia mpaka wa Kabanga, mkoani Kagera, mnamo tarehe 22 Novemba 2025.
Aidha Mtuhumiwa Shadia Japhari Majaliwa, miaka 18, raia wa Burundi na mkazi wa Kisuru, alikamatwa katika eneo la Nyatukara wilayani Sengerema akiwa ndani ya gari aina ya Yutong lenye namba za usajili T 131 DRE.
Magari yote mawili yamekamatwa na dereva pamoja na wasaidizi wengine wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na tuhuma za kuwasafirisha raia hao wa Burundi.
Kamanda Mutafungwa amesema kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha doria na vizuizi vya barabarani kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama na wananchi ili kudhibiti matukio ya kihalifu.
Aidha, amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwafichua wahalifu popote walipo, ili waweze kudhibitiwa kabla hawajafanya uhalifu wowote.