Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itawalipa fidia wote waliopisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo leo Januari 06, 2026wakati wa hafla ya ufunguzi wa Barabara ya Juu (Flyover) ya Dk Hussein Ali Mwinyi – Mwanakwerekwe, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa Serikali imeunda Kamati Maalumu ya uhakiki na tathmini ya fidia maeneo yaliyopitiwa na miradi ya maendeleo, ili kila mwananchi analipwa stahiki yake kwa haki na kwa mujibu wa sheria.
Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa ujenzi wa barabara, madaraja na flyover unaongeza thamani ya ardhi na nyumba, hivyo ni muhimu wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Amesema ujenzi wa Flyover hiyo ni ushahidi wa dhana ya uongozi unaoacha alama, nakuwataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo na kuacha kujenga maeneo ya hifadhi ya barabara kwa ajili ya uduma za kijamii ikiwemo maji na umeme.
Zanzibar huadhimisha kilele cha siku ya mapinduzi Januari 12 ya kila mwaka na mwaka huu inaadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu Januari 12 mwaka 1964 na mwaka huu yanaadhimishwa chini ya Rais na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi ya Zanzibar Rais Dkt Hussen Aly Mwinyi.