
Rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy (70), amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya ufadhili haramu wa kampeni za urais mwaka 2007, kwa kutumia fedha kutoka kwa serikali ya aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi.
Hukumu hiyo ya hatia inamaanisha kuwa Sarkozy, aliyeongoza Ufaransa kati ya mwaka 2007 na 2012 na alistaafu siasa rasmi mwaka 2017, atalazimika kutumikia kifungo hicho hata kama atakata rufaa.
Sarkozy alishtakiwa kwa kufanya makubaliano na Gaddafi mwaka 2005, alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ili kupata ufadhili wa kampeni yake kwa kubadilishana na kumuunga mkono Gaddafi katika jukwaa la kimataifa, wakati Libya ilikuwa ikitengwa na mataifa mengine.
Rais huyo wa zamani amekana mashtaka yote na kudai kuwa kesi hiyo ina msukumo wa kisiasa.
Sarkozy tayari ametangaza kuwa atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, aliyoielezea kama nzito mno kwa utawala wa sheria.
Akizungumza baada ya kusikiliza hukumu hiyo leo Alhamisi, Septemba 25, 2025, amedai kesi hiyo ina msukumo wa kisiasa, huku upande wa waendesha mashtaka ukidai Sarkozy aliahidi kumsaidia Gaddafi kurekebisha sifa yake mbaya mbele ya mataifa ya magharibi kama malipo ya msaada huo wa kifedha.
Katika unafuu mdogo kwake, Mahakama ya Jinai ya Paris iliagiza kuwa, Sarkozy asiwekwe rumande kwanza na waendesha mashtaka wamepewa muda wa mwezi mmoja kumjulisha lini ataanza kutumikia kifungo chake.