
Serikali imetoa zaidi ya Shilingi milioni 126 kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika ajali ya magari mawili yaligongana uso kwa uso na kuwaka moto Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ambapo kila familia imepewa Shilingi milioni 3 kwa ajili ya taratibu za maziko.
Pamoja na kupewa fedha hizo, Serikali imegharamikia majeneza pamoja na kusafirisha miili hiyo kwa ajili ya taratibu za maziko wilayani Same.
Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi Kampuni ya Chanel One, lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso kisha kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.
Waliofariki katika ajali hiyo ni watu 42, ambapo kwenye gari dogo aina Coaster walifariki watu 31 waliokuwa wanakwenda harusini mjini Moshi, huku kwenye basi la Chanel One wakifariki watu 11.
Shughuli ya kuaga miili hiyo, inaendelea katika viwanja vya hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu pamoja na viongozi wengine wa Serikali.