
Serikali imetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi wa Mitaa ya Nyakabale na Nyamalembo katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita, ili kupisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML). Hatua inayoleta suluhu ya mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 26.
Akizungumza Mkoani Geita, Waziri wa Madini, Mhe.Anthony Mavunde, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikifuatilia kwa karibu changamoto za wananchi wa Geita na kutoa maelekezo mahsusi kuhakikisha zinatatuliwa kwa ufanisi.
Amesema kuanzia leo Agosti 22, 2005, timu ya wataalamu wa Serikali itaanza kazi ya uthamini wa mali, na ndani ya siku 40 tathmini hiyo itakamilika ili wananchi waweze kulipwa stahiki zao.
Aidha, Waziri ameeleza kuwa, mgogoro huo ulikuwa na hoja 13 za msingi ambazo zilihitaji kushughulikiwa, ambapo ndani ya mwaka mmoja na miezi mitatu Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kutatua hoja 10 kati ya hizo na hatimaye leo kutatua hoja nyingine mbili.
Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, katika jitihada hizo, GGML imekubali kurekebisha mipaka yake ya leseni ya uchimbaji lna kuliachia eneo linalobaki kwa ajili ya wakazi wa maeneo hayo.
Pia, Waziri Mavunde ametumia nafasi hiyo kuwaonya na kuwakumbusha wananchi kuepuka tabia ya ‘tegesha’ kwani inaweza kukwamisha zoezi la tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaostahili kupata haki zao kwa wakati na kuleta usumbufu kwa mwekezaji na wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kufuatilia kwa karibu mgogoro huo wa muda mrefu, na kumpongeza Waziri Mavunde kwa kusimamia utekelezaji kwa umakini.