
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itahakikisha inawalinda na kuwapatia fursa stahiki Watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye ualbino katika ujenzi wa Taifa.
Majaliwa ameyasema hayo leo wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika uwanja wa Mwanga Centre, mkoani Kigoma.
Amesema katika kutekeleza mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, hadi kufikia Machi, mwaka huu tayari shilingi bilioni 5.48 zimetolewa kwa vikundi 891 vya Watu Wenye Ulemavu nchini.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha ustawi na utoaji huduma kwa watu wenye ualbino ikiwemo kuwatambua, kuimarisha mifumo ya kisera na kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu hapa nchini.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa kupitia maadhimisho hayo, Serikali imezindua programu janja ‘Albino Mobile App’ ambayo itawezesha kufanya usajili na ukusanyaji wa taarifa za watu wenye ualbino kwa njia ya kidigitali.
Amesema kuwa mfumo huo utarahisisha, utaharakisha na utahakikisha usahihi katika usajili wa watu wenye ualbino na ulemavu nchini Tanzania, hususan walioko maeneo ya pembezoni.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS) Godson Mollel Amesema kuwa Serikali imefanya mambo makubwa yenye lengo la kuwawezesha watu wenye Albino nchini ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kununua mafuta kinga ambayo hugawiwa bure.