
Serikali imesema imewekeza nguvu kubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), vyombo vya ulinzi na usalama, wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na jamii kwa ujumla, ambapo imepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa katika kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa hizo hatarishi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 23, 2025, katika Ukumbi wa Jengo la Habari bungeni, wakati akitoa taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amesema kuwa kwa mwaka 2024, bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi, ambapo jumla ya tani 2,307.37 zilikamatwa.
Amesema kati ya tani hizo, tani 2,303.2 ni bangi iliyozalishwa nchini na tani 4.17 ni bangi yenye kiwango cha juu cha kemikali ya THC maarufu kama skanka, iliyoingizwa nchini kutoka katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika.
Lukuvi amesema kwa upande wa dawa za kulevya zinazozalishwa viwandani, Serikali ilifanikiwa kukamata tani 1.7 za methamphetamine, kilo 433.02 za heroin na gramu 853 za cocaine. Kwa mara ya kwanza, Serikali pia ilikamata kilo tano za dawa mpya ya kulevya inayojulikana kama methylene-dioxy-pyrovalerone (MDPV), ambayo ilikuwa ikiingizwa nchini.
Aidha, Waziri amewasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapohisi au kushuhudia viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya kwa vyombo husika ili kuifanya nchi ya Tanzania kuwa mahali salama na huru dhidi ya matumizi na biashara ya dawa hizo.