
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendeleza juhudi za kuwawezesha wavuvi wa Mkoa wa Kagera kufanya uvuvi wa kisasa kwa kuwapatia mafunzo, mikopo ya mitaji na vyombo vya kisasa vitakavyowawezesha kufika mbali zaidi majini.
Katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika leo Alhamisi, Oktoba 16, 2025, kwenye Viwanja vya Kaitaba, Bukoba Mjini, Dkt. Samia ameeleza kuwa serikali yake itajielekeza katika kuongeza tija na uzalishaji kwenye sekta ya uvuvi kupitia mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), ambao unalenga kuwawezesha vijana na wavuvi wengi zaidi kujihusisha na ufugaji wa samaki kwenye vizimba.
Amesema ahadi hiyo inalenga kukabiliana na changamoto ya upungufu wa samaki katika maziwa mbalimbali nchini, sambamba na kuongeza kipato cha wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi kama chanzo kikuu cha maisha.
Katika sekta ya mifugo, Dkt. Samia ameahidi kuendeleza kampeni ya kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kupitia chanjo, ruzuku na utambuzi wa mifugo, hatua itakayosaidia wafugaji kuzalisha mifugo bora na yenye viwango vya kimataifa.
Aidha, amesema serikali yake itahakikisha ujenzi wa machinjio ya kisasa unaotekelezwa unakamilika kwa wakati ili kuboresha huduma, kuongeza thamani ya bidhaa za mifugo na kuwezesha bidhaa hizo kuuzika katika soko la kimataifa.
Halikadhalika Dkt. Samia ameahidi kusimamia kukamilika kwa ujenzi wa tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mkoani Kagera, ambalo limefikia asilimia 70 ya utekelezaji huku akibainisha kuwa serikali yake itaendelea kuimarisha mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ili kila Mtanzania mwenye sifa apate nafasi ya kusoma vyuo vikuu bila kujali hali ya kifedha ya familia yake.
Pia ameahidi kuendeleza sera ya elimu bure kuanzia shule za msingi hadi kidato cha sita, sambamba na kuharakisha ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari, hususan zile zilizopo katika maeneo ya visiwani mkoani Kagera.
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu ndani ya kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, Dkt. Samia amesema mkoa wa Kagera umenufaika kwa kujengwa shule tatu mpya za amali, shule moja ya sekondari ya sayansi kwa wasichana, pamoja na vyuo vitano vya VETA, ikiwemo chuo cha VETA cha mkoa kilichopo Burugo, wilayani Bukoba.