
Serikali mkoani Kagera imewataka wakulima wa Kahawa kuboresha mashamba yao ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Akizungumza na wadau wa Kahawa mkuu wa mkoa huo Hajat Fatma Mwasa amesema kuwa uzalishaji wa zao hilo umekuwa haukui na kupelekea kubaki kati ya tani elfu 50 na 60 na kwamba inatokana na matumizi ya pembejeo zisizo bora sambamba na kutokuwepo maboresho ya mashamba.
Amesema kuwa mbali na mkoa wa Kagera kuchangia asilimia 60 ya kahawa zote zilizokusanywa bado zinatakiwa kufanyika jitihada za kuhakikisha uzalishaji unaongezeka ikiwa ni pamoja na wakulima kuboresha maeneo yenye changamoto kwao.
Nao baadhi ya wakulima wa kahawa wilayani Bukoba akiwemo Mugisha Jovine na Emelensiana Ananias wamekiri asilimia kubwa ya wakulima kuwa na mashamba yaliyolimwa kwa muda mrefu pia wamekishukuru chama kikuu cha ushirika na serikali kuja na kampeni za ufufuaji wa mashamba hayo.