
Serikali imekanusha madai ya kuwepo kwa njama ya kumwekea sumu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye kwa sasa yuko rumande akisubiri uamuzi wa mashauri yake mahakamani.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, leo Serikali imezitaja taarifa zinazosambazwa juu ya madai hayo kuwa ni za uzushi, na zisizo na msingi wowote.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa Serikali haijawahi kuwa na mpango wa kumdhuru mtu yeyote aliyeko kizuizini na kwamba taarifa hizo ni sehemu ya kampeni ovu ya kuchafua sifa ya Tanzania kimataifa.
Lakini kabla ya taarifa hiyo ya serikali, Chama cha CHADEMA Kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, kilisema kilikuwa kimetoa taarifa rasmi hapo jana Julai 2 kikieleza wasiwasi wake kuhusu usalama wa mwenyekiti wake Tundu Lissu.:
Kwa mujibu wa CHADEMA, wanataka uchunguzi huru ufanyike na pia Serikali iwajibike kuhakikisha usalama wa Lissu akiwa rumande, huku wakitoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufuatilia kwa karibu suala hilo.