
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amekabidhi Magari pamoja na Vifaa vya Uokozi kwa Jeshi la Zimamoto na na Uokozi Mkoani humo.
Akiongea katika hafla ya kukabidhi vifaa na magari hayo sita iliyofanyika leo tarehe 21 Oktoba, 2025 katika viwanja vya ofisi ya jeshi hilo Jijini Mwanza Mtanda amesema serikali inaonesha kwa vitendo kiu ya kumaliza changamoto za uokozi kwa haraka hivyo jeshi hilo lina wajibu na dhamana ya kuvitunza vifaa hivyo.
“Tufuate kanuni na taratibu za jeshi letu kuhakikisha magari na vifaa hivi vinafanya kazi zilizokusudiwa na si vinginevyo, madereva na wasimamizi wa vyombo hivi wahakikishe wanavitunza vizuri”.
Amesema, miaka ya nyuma jeshi hilo halikuaminika na wananchi kwa kuchelewa kwenye majanga hususani ya moto lakini kwa sasa serikali inahakikisha inaboresha miundombinu pamoja na rasilimali muhimu kwenye jeshi hilo ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Kadhalika, amelitaka jeshi hilo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajue huduma zonazotolewa sambamba na kuwataka wawe wazalendo wenye kutumia namba 114 kwa ajili ya kuomba msaada wanapopata dharula na sio kuitumia kwa sababu za mzaha.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Elisha Kamugisha kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia vifaa hivyo ambapo amebainisha kuwa vitasaidia kuboresha kazi na kusogeza huduma kwa jamii.
Magari yaliyokabidhiwa ni Mobile Workshop (Gari litakalotumika kama karakana), Command Car (Gari litakalotumika katika kusimamia dharura), Ambulance 2 (Gari za kubebea wagonjwa), Gari dogo la utawala na Rescue Van (Gari litakalotumika kwenye shughuli za uokozi nchi kavu).