Na Clement Shawishi- Geita
Serikali imeendelea kuongeza juhudi za kupambana na udumavu kwa watoto kwa kuzindua programu jumuishi ya lishe mahususi katika mikoa ya Geita, Tabora na Iringa inayolenga kuboresha afya na ukuaji wa watoto chini ya miaka mitano.
Akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo uliofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Profesa Riziki Shemdoe ameagiza Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Geita kuhakikisha Maofisa Maendeleo ya Jamii wanapatiwa usafiri ili waweze kufikia wananchi kwa urahisi zaidi.

Profesa Shemdoe pia amesisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii pamoja na kuhakikisha takwimu sahihi zinakusanywa ili kusaidia utekelezaji mzuri wa programu hiyo inayofadhiliwa na Taasisi ya Big Win Philanthropy ya nchini Uingereza.
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya afya Profesa Tumaini Nagu amesema programu hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubishi, kuimarisha malezi bora ya mtoto na kuondoa mila na desturi zinazoathiri lishe ya watoto.
Kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Tabora na Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela ameahidi ushirikiano wa karibu na taasisi inayofadhili programu hiyo ili kuhakikisha malengo ya kupunguza udumavu yanafikiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Bi Husna Toni akizungumza kwa niaba ya wanufaika amesema halmashauri yao itaendelea kushirikiana na wataalam wa lishe ili kuhakikisha mafanikio ya programu hiyo yanaonekana katika jamii.

Programu hiyo inatekelezwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni mbili na kwa sasa imeanza katika mikoa ya Geita, Tabora na Iringa.
