Na Clement Shawishi- Geita
GEITA: Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amewataka viongozi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, Jeshi la Zimamoto na wananchi kwa ujumla kutunza na kulinda mali za Umma kwa manufaa ya jamii.
Shigela amesema hayo jana Februari 09, 2026 baada ya kupokea na kukabidhi rasmi gari la zimamoto na uokoaji katika mamlaka ya mji mdogo wa Katoro lililotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Amesema gari hilo ni mahususi kusaidia kuzima ajali za moto Katoro na maeneo jirani hivyo halitakiwi kutumika kinyume na ilivyokusudiwa pia wananchi wanatakiwa kujenga nyumba zinazoruhusu gari hilo kupita.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita ASP Kenneth Mwakasitu amesema gari hilo ni la kisasa lenye uwezo wa kubeba lita 500 za maji pia kutumika katika shughuli mbalimbali za zimamoto na uokoaji wakati wa majanga tofauti.
Mbunge wa Jimbo la Katoro Mhandisi Kija Limbu Ntemi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Jumanne Misungwi wamesema ujio wa gari hilo ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma za uokoaji na zimamoto ambazo kwa muda mrefu wananchi wa Katoro walizitegemea kutoka Geita mjini
Wananchi wa Katoro waliohudhuria hafla hiyo wamepongeza hatua ya serikali kupeleka gari hilo, wakimpongeza Mbunge wa Jimbo la Katoro kwa jitihada zake za kuwasilisha kero zao Bungeni na kuanza vyema kazi ya uwakilishi kwao.
