Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali imetoa shilingi trilioni 1.319 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu hadi kufikia Machi 2026, ikiwa ni asilimia 72.80 ya bajeti iliyoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti pamoja na makadirio ya mwaka 2026/2027 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Machi 23, 2026 mkoani Dodoma, Ulega alieleza kuwa fedha hizo zimewezesha kupatikana kwa mafanikio mbalimbali katika sekta ya ujenzi.
Katika sekta ya barabara, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umekamilisha ujenzi wa kilometa 206.33 za barabara kwa kiwango cha lami pamoja na madaraja makubwa manne.
Pia, miradi 76 kati ya 81 ya dharura ya ujenzi wa madaraja yaliyoathiriwa na mvua za El NiΓ±o imekamilika.

Aidha, ujenzi wa madaraja muhimu ukiwemo Pangani, Jangwani, Mbambe, Sukuma, Simiyu, Mirumba na Mitomoni unaendelea katika hatua mbalimbali.
Kwa upande wa viwanja vya ndege, Ulega amesema awamu ya kwanza ya uboreshaji wa viwanja vya Tabora na Iringa imekamilika, huku ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato ukifikia asilimia 83.
Viwanja vya Sumbawanga na Shinyanga vimefikia asilimia 95 kila kimoja, Musoma asilimia 67, na Kigoma asilimia 42.
