Wizara ya Afya imetoa tahadhari kwa wananchi kufuatia kuongezeka kwa wagonjwa wa mafua makali ya Influenza na UVIKO-19, huku ikionya pia kuhusu hatari ya homa ya dengue katika kipindi hiki cha mvua.
Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Maghembe, leo Februari 25, 2026, imeeleza kuwa Wizara imeendelea kufuatilia mwenendo wa magonjwa ya mlipuko na kubaini kuwa kila mwaka, kuanzia Novemba hadi Aprili, kumekuwa na ongezeko la maambukizi ya mafua makali ya Influenza na UVIKO-19 nchini na duniani.
Magonjwa hayo huenea kupitia majimaji yanayotoka kwa mgonjwa wakati wa kukohoa, kupiga chafya au kuzungumza, pamoja na kugusa nyuso zilizochafuliwa.
Dalili zake ni pamoja na homa kali, kikohozi, maumivu ya kichwa na mwili, mafua, kuwashwa koo, na uchovu.

Mganga Mkuu wa Serikali amewataka wananchi kuchukua tahadhari mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufunika pua na mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, kuepuka misongamano isiyo ya lazima, kuvaa barakoa ukiwa na dalili au ukiwa karibu na mgonjwa, kuzingatia usafi binafsi na wa mazingira, na kuwahi vituo vya afya kupata matibabu stahiki huku kuepuka kutumia antibiotiki bila ushauri wa wataalamu.
Aidha, Wizara imekumbusha kuhusu homa ya dengue inayosababishwa na mbu aina ya Aedes, ambao huuma zaidi asubuhi, mchana na jioni.
Dalili zake ni homa kali, maumivu ya kichwa, viungo na macho pamoja na uchovu.
