Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewataka Watanzania wanaoishi katika nchi za Mashariki ya Kati kuwa waangalifu na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka za nchi husika, baada ya kuzorota kwa hali ya usalama katika ukanda huo.
Tahadhari hiyo inakuja baada ya mapigano makali ya makombora kati ya Iran na Israel, kufuatia kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran, Ali Khamenei, kilichoripotiwa Februari 28, 2026 baada ya shambulizi la Marekani na Israel.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya tukio hilo Iran na Israel zimekuwa zikirushiana makombora, wakati Iran ikishambulia maeneo yanayohusishwa na kambi za kijeshi za Marekani katika nchi mbalimbali za ukanda huo ikiwemo Bahrain, Kuwait, Qatar, Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, kulipiza kisasi cha mauaji ya Kiongozi huyo.
Hali hiyo imezua hofu kubwa ya kiusalama kwa Iran na Israel, lakini pia katika ukanda mzima wa Mashariki ya Kati kutokana na majibizano hayo ya kijeshi.
Taarifa iliyotolewa Machi 3, 2026, wizara hiyo imewataka Watanzania waliopo katika ukanda huo kuepuka safari zisizo za lazima za kwenda au kutoka Mashariki ya Kati kwa kipindi hiki, na kubaki katika makazi yao kadri inavyowezekana.
