Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imezindua tawi jipya ndani ya Soko Kuu la Kariakoo mkoani Dar es Salaam, kusogeza karibu huduma za kibingwa za moyo na huduma nyingine za afya kwa wafanyabiashara na wananchi wa eneo hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa JKCI, Dkt. Hassan Mshinda, amesema hayo wakati wa ufunguzi wa tawi hilo Februari 24 2026 hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo na kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi wanaofanya shughuli zao Kariakoo.
Tawi hilo litatoa huduma za uchunguzi wa awali wa magonjwa ya moyo, ushauri wa kitabibu na huduma nyingine za afya kwa wafanyabiashara na wakazi wa Kariakoo.
Dkt Mshinda amesema “Afya ni mtaji bora kuliko yote. Ili kuhakikisha tunalinda mtaji wa wafanyabiashara na wakazi wa Kariakoo, Serikali kupitia JKCI imewekeza katika miundombinu, wataalamu waliobobea na vifaa vya kisasa ili kuhakikisha uchunguzi na matibabu, ikiwemo ya magonjwa ya moyo, yanapatikana katika tawi la Kariakoo. Kaulimbiu yetu ni ‘Daktari mkononi mwako, linda afya endeleza biashara Kariakoo,’”
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema tawi hilo litawahudumia wananchi wote, wenye matatizo ya moyo na hata wasiokuwa nayo, kwa kutoa huduma mbalimbali za kitabibu.
Ameongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja zimewekezwa katika ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo mashine zinazotumia teknolojia ya akili bandia (AI) kupima afya ya moyo na umeme wa moyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kisenge, mfanyabiashara atakapopata tatizo akiwa eneo la kazi atampigia daktari simu na kupata ushauri wa haraka kupitia huduma za tiba mtandao.
Aidha, wagonjwa watakaogundulika kuwa na matatizo wataendelea kufuatiliwa hata wakiwa nyumbani kwa kutumia teknolojia ya akili bandia kupitia kifaa maalumu kinachowekwa chini ya godoro, kitakachofuatilia mapigo ya moyo, kiwango cha oksijeni na presha ya damu.
