
Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mtahabwa, amesema Tanzania ipo katika zama za mageuzi makubwa ya elimu, yakijikita kwenye Sera ya Elimu ya 2014 (Toleo la 2023) na mitaala mipya kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.
Amesema mabadiliko hayo yanalenga kutoa elimu yenye maarifa, ujuzi na maadili ili kumkomboa mtanzania katika nyanja zote za maisha.
Dkt. Mtahabwa ameyasema hayo leo, Agosti 21, 2025, katika mdahalo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuhusu ujuzi stahiki kwa vijana balehe walio nje ya mfumo rasmi.
Amesema mdahalo huo unalenga kupokea maoni ya vijana ili kusaidia kuboresha miongozo ya elimu na kuhakikisha inawasaidia kujiajiri na kuwaajiri wengine kulingana na muktadha wa kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake Jeremia Pius kutoka Shule ya Sekondari Kijitonyama amesema mdahalo huo umewasaidia vijana kujijenga kitabia na kutambua fursa.
Nae Mariam Fidelis kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VTC) amesema amejifunza kujitambua na kuepuka makundi hatarishi, ili aweze kuelimisha wengine katika jamii.