Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema Tanzania imejizatiti katika kuendeleza nishati ya jotoardhi, ili kuhakikisha nchi inakuwa na nishati ya kutosha, nafuu na endelevu inayotokana na vyanzo mchanganyiko.
Ndejembi amesema hayo Januari 12, 2026 kwenye Baraza la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) katika Mkutano wa Mwaka wa Muungano wa Kimataifa wa Jotoardhi (GGA), unaofanyika jijini Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.
Amesema ili kutekeleza dhamira hiyo serikali imeweka mipango ya uzalishaji wa umeme wa jotoardhi katika Dira ya Maendeleo 2050, Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) na Mkataba wa Nchi kuhusu Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi (NDCs).
Aidha ameongeza kuwa Tanzania pia kupitia Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi (TGDC) inaendeleza maeneo kadhaa ya kipaumbele ya jotoardhi, ikiwemo Ngozi Songwe, Kiejo-Mbaka), Natron na Luhoi ,huku lengo likiwa ni kuwa na mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme wa megawati 130, ifikapo 2030 ambapo mtambo huo utaanza kwa kuzalisha megawati 30.
Hata hivyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono malengo ya dunia kuelekea kwenye uzalishaji wa umeme unaotokana na nishati safi.