
Kampuni ya Tembo Nickel imethibitisha ratiba ya kuanza rasmi ujenzi wa Mgodi wa Kabanga Nickel uliopo wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera ifikapo Oktoba, 2025.
Hayo yamesemwa leo Jumatato na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Lifezone Metals inayomiliki kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited kwa ubia na Serikali ya Tanzania, Chris Showalter, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Kabanga Nickel.
Aidha Showalter amesema Sambamba na ujenzi wa mgodi huo, kampuni inaendelea kuthibitisha mpango wake wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kusafisha madini ya Nickel kwa kuyaongezea thamani ndani ya nchi
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mradi wa Kabanga Nickel unategemewa kuleta mapinduzi katika kuchochea uchumi na maendeleo ya nchi yetu.
Serikali imetoa wito kwa kampuni zote kuhakikisha zinaanza mara moja shughuli za uendelezaji miradi ya madini kama ilivyoainishwa kwenye sheria ya madini sura ya 123, ni muhimu sheria kuzingatiwa katika utekelezaji wa miradi ili miradi hii ilete tija kwa jamii na kwa Taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde amesisitiza kampuni zote zenye Leseni za kati na kubwa kuhakikisha maeneo yao yanaendelezwa kwa mujibu ya masharti ya leseni zao.