
Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini Thabo Mbeki amewasili nchini Tanzania Mei 20, 2025, kushiriki Mhadhara wa Siku ya Afrika yaani Africa Day Lecture.
Mhadhara huo umeandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, ambao utafanyika jijini Dar es Salaam Mei 24, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Thabo Mbeki amepokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato David Chumi.
Mhadhara huo ni wa 15 kuandaliwa na Taasisi ya Thabo Mbeki, unatarajiwa kujadili kuhusu mustakabali wa Bara la Afrika na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wanataaluma, wadau kutoka Serikalini, viongozi wastaafu, vijana, na wawakilishi wa sekta binafsi.
Aidha Rais Mstaafu Mbeki anatarajiwa kushiriki katika mijadala mbalimbali ikiwemo; mjadala kuhusu Uchumi wa Buluu na Utalii, mjadala wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu, halikadhalika majadiliano kuhusu Fursa ya Urais wa Afrika ya Kusini wa kundi la Nchi zenye Uchumi Mkubwa Duniani (G20) kwa ustawi na maendeleo ya Afrika.
Mhadhara wa Siku ya Afrika unafanyika nchini baada ya Taasisi ya Thabo Mbeki kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji kwa ukanda wa Afrika Mashariki.