Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa serikali imebaini watumishi wa umma 7,447 wanapokea mishahara isiyoendana na majukumu wanayofanya, na kusababisha kuwepo kwa tofauti kubwa ya mishahara kati ya watumishi wa umma na ile inayolipwa katika sekta binafsi.
Waziri Mkuu ameeleza hayo leo April 1, 2026 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, na kubainisha kuwa hadi Machi 26, mwaka huu, watumishi hao wamelipwa mishahara ya binafsi yenye gharama ya shilingi bilioni 14.34.
Dkt. Nchemba amesema Serikali imeona ni lazima kuchukua hatua ya kupunguza tofauti ya viwango vya mishahara katika utumishi wa umma na sekta binafsi pamoja na kuwianisha mishahara ya watumishi wa umma ili kuepuka upungufu na kuhakikisha malipo yanalingana na kazi zinazofanywa.
Ameongeza kuwa serikali itahuisha sheria ya utumishi wa umma pamoja na kanuni zake kuhusu utoaji wa kibali cha mishahara binafsi, pamoja na waraka unaohusu watumishi wanaobadilishwa kazi ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema mapitio ya waraka kuhusu utaratibu wa kushughulikia maombi ya mishahara binafsi kwa watumishi wa umma yatafanywa ili kuboresha uwazi na ufanisi.
