Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Sudan Kusini (SSRA) zinatarajia kuanzisha ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kodi ikiwemo kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi baina ya mamlaka hizo mbili.
Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja baina ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda na Kamishna Mkuu wa SSRA Bw. William Anyuon Koul kilichofanyika leo Januari 22, 2026 katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mwenda amesema miongoni mwa maendeo watakayoshirikiana ni kudhibiti ukwepaji kodi kwa kuweka udhibiti wa mizigo inayosafirishwa kupitia Bandari za Tanga na Dar es Salaam kuelekea Sudan Kusini.
Amesema Sudan Kusini inalenga kutumia kikamilifu Bandari za Dar es Salaam na Tanga kupitisha mizigo yao na wameomba kutengewa eneo maalum la forodha kwa ajili ya kusimamia mizigo yao na kuhakikisha inafika kwa wakati na kwa usalama.

Amesema ili kufanikisha hilo wamekubaliana kujenga mfumo wa pamoja baina ya SSRA na TRA ili kuwezesha mifumo yao kusomana kwa lengo la kudhibiti mapato na kuziba mianya ya rushwa jambo ambalo litakuwa na manufaa kwa nchi zote mbili.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa SSRA Bw. William Anyuon Koul amesema ushirikiano baina yao na TRA utaiwezesha Sudani Kusini kutumia bandari za Dar es Salaam na Tanga na kudhibiti ukwepaji wa mapato kupitia mifumo kusomana.