
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema linabadili namna linavyojiendesha kutoka kusimamia kila kitu lenyewe hadi kushirikisha sekta binafsi ili kuongeza ufanisi na mapato.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa amesema mabadiliko hayo yanatokana na mageuzi ya mashirika ya umma yanayoendelea kufanywa na Serikali, ambayo yanahimiza ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi.
Amesema kuwa changamoto kubwa ya shirika hilo ni kuwa na miundombinu mikubwa inayotumika kwa theluthi moja pekee ya uwezo wake. Hali hiyo, amesema, inahitaji mabadiliko ya kimuundo ambapo sekta binafsi itaingia kutumia sehemu iliyosalia na kuisaidia TRC kujiendesha kibiashara zaidi.
Shiwa ameeleza kuwa kwa sasa TRC inajiandaa kushirikisha sekta binafsi katika maeneo ya ukarabati wa njia za reli, vichwa na mabehewa, huku shirika likibaki na jukumu kuu la uendeshaji.