
Ripoti kutoka vyanzo vya karibu na Ikulu ya Marekani zinaeleza kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump anafikiria kupunguza adhabu ya kifungo cha rapa na mfanyabiashara Sean “Diddy” Combs mapema wiki hii.
Kwa mujibu wa maafisa wa ngazi ya juu walionukuliwa na vyombo kadhaa vya habari ikiwemo Hindustan Times na Complex, baadhi ya washauri wa Trump wamepinga uamuzi huo, lakini chanzo kimoja kilisema wazi kuwa, Trump atafanya anachotaka.
Diddy alihukumiwa kifungo cha miezi 50 mapema mwezi Oktoba mwaka huu kwa makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa Mann Act, sheria ya usafirishaji kwa nia ya biashara isiyofaa, na ameshatumikia takriban miezi 13. Timu yake ya wanasheria imeripotiwa kuwasiliana na maafisa wa Ikulu kuomba msamaha au kupunguziwa adhabu.
Hadi sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa na Trump wala Ikulu kuthibitisha au kukanusha taarifa hizi. Hata hivyo, endapo itatokea, itakuwa ni mojawapo ya maamuzi ya utata zaidi kwenye historia ya msamaha wa rais nchini Marekani, ikizingatiwa hadhi ya Diddy kwenye muziki na biashara.