
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoa wa Geita inaendelea na uchunguzi kwa baadhi ya wagombea ubunge na udiwani pamoja na wajumbe kuhusiana na tuhuma za vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kabla na baada ya kura za maoni ndani ya chama cha mapinduzi CCM
Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Geita James Ruge amesema hayo leo Agosti 14,2025 wakati akitoa taarifa kwa wandishi wa habari za utendajikazi wa taasisi kwa kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi June 2025
Ruge amesema ufuatiliaji wa tukio hilo ulianza bada ya kuonekana kwa picha mjongeo mnamo Agosti 2 na kuhusisha wajumbe kutoka umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi CCM kata ya Nyankumbu jimbo la Geitamjini wakigawana fedha
Amesema baada ya kipande hicho cha picha mjongeo, watu hao walitambuliwa na kukamatwa kwa mahojiano ya tuhuma hizo
Ruge amesema tukio lingine linahusisha picha mjongeo la Agosti 4 siku ya uchaguzi wa ndani ya chama ambapo wajumbe wa jimbo la Chato Kaskazini kijiji cha Buzilayombo walionekana wakiwa pamoja katika tukio la kula chakula na vinywaji ambavyo vilikuwa vimeandaliwa kwa wajumbe na wote waliokamatwa waliachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea wa tuhuma hizo
Pia TAKUKURU Geita imeweza kurejesha kiasi cha shiligi milioni 770 kutoka vyama vya ushirikia vya kilimo cha tumbaku wilayani Mbogwe ambavyo vilikuwa vimeshindwa kurejesha ikiwa ni mikopo ambayo vilikopa kutoka benki ya NBC tawi la Kahama pamoja na benki ya CRDB Mbogwe
Vyama hivyo vya msingi vya ushirika vya kilimo cha tumbaku wilaya ya Mbogwe vilikuwa vimeshindwa kurehjesha mikopo hiyo ambapo TAKUKURU iliweza kufanya uchambuzi wa mifumo katika vya msingi na vikuu vya ushirika na kubaini kutorejeshwa kwa dola za kimarekani 341,137/= ambazo ni sawa na Sh. 930,928,759 fedha za kitanzania.